MAISHA YAKO YA USTAWI KATIKA KRISTO
Na Mungu aweza kuwajaza neema za kila namna (kila aina ya riziki na baraka za kidunia) kuja kwenu kwa wingi, ili daima na katika hali zote na hitaji liwalo lote lile muwe na ziada [mkimiliki vingi vya kuzidi hata kutosheleza kutohitaji hisani yo yote au kusaidiwa, mkiwa na nakshi katika utele kwa ajili ya kila kazi njema na kutoa misaada mbalimbali] (2 CORINTHIANS 9:8 “AMPC”).
Mpango wa Mungu ni kwamba watoto Wake wawe na riziki tele (ugavi endelevu). Nimeyachunguza Maandiko na sioni mahali yanatupa wazo kwamba umaskini, ukosefu na uhitaji vinaweza kuwa ni mapenzi ya Mungu; hakuna hata pendekezo la suala hilo katika Biblia. Kumbuka kwamba hata ibilisi alimlaumu Mungu kwa kumfanya Ayubu kuwa tajiri, na kumbariki kwa mali nyingi (Ayubu 1:9-10).
Unapaswa kukumbatia uhalisia kwamba ustawi wako wa kifedha au mali ni muhimu kwa Mungu. Alisema katika 3 Yohana 1:2, “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.” Fikiria kuhusu hilo!
Kisha Ayubu 22:24-25 “KJV” inasema, “Ndipo utalaza dhahabu kama mavumbi…nawe utakuwa na fedha tele.” Ikiwa umewahi kufuta vumbi kwenye meza, utaona kwamba baada ya kitambo, vumbi litakuja tena juu ya meza. Inatoa taswira ya aina ya mafanikio ambayo watu wa Mungu wameitwa kupata—ugavi usio na mwisho na mwingi.
Inatukumbusha maneno ya Daudi katika Zaburi 23:1-2, “Bwana ndiye mchungaji wangu; sitapungukiwa na kitu. Hunilaza katika malisho ya majani mabichi…” Hiyo ndiyo njia ya kufikiri. Umechomekwa kwenye mkondo wa usambazaji usioisha. Hii haina uhusiano wowote na nchi unayoishi; ni maisha uliyoitiwa katika Kristo Yesu.
Kumbuka tena yale tuliyosoma katika andiko letu la ufunguzi. Mungu hataki wewe uwe na fikira za uhitaji. Wewe ni mrithi wa Mungu, na mrithi sawasawa na Kristo (Warumi 8:17). 1 Wakorintho 3:21 inasema, “… vitu vyote ni vyenu…” Baba yako wa mbinguni Anamiliki ulimwengu wote na amekupatia wewe yote kwa sababu wewe ni uzao wa Ibrahimu: “Na ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi” (Wagalatia 3:29).
Chagua maisha ya furaha na mafanikio katika Kristo. Usione kazi yako au biashara kama chanzo chako cha riziki, bali kama njia ya kuwabariki wengine. Katika Kristo, umeletwa katika maisha ya utele; tambua na furahia urithi wako.
SALA
Baba Mpendwa, wewe ni mwenye neema na fadhili. Ninakushukuru kwa kunifanya sawa-sawa na Kristo; dunia ni mali yangu. Ninachagua kuishi maisha ya furaha na mafanikio katika Kristo, kwa kuwa vitu vyote ni vyangu, na hakuna kitu kizuri ambacho nimezuiliwa. Ninaishi katika ulimwengu wa utele na maisha yangu ni udhihirisho wa upendo Wako na neema Yako, katika Jina la Yesu. Amina.
Author: Mwalimu Alex Mushi