Ufufuo ndio ufunguo

 


UFUFUO NDIO UFUNGUO

“Lakini yanenaje?…Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka” (WARUMI 10:8-9).

Ukristo huanza na ufufuo wa Yesu Kristo, sio kifo. Hii haimaanishi kifo cha Yesu Kristo si cha muhimu, kwa maana kusingekuwa na ufufuo kama kusingekuwa na kifo. Ikiwa unaamini ufufuo, bila shaka unaamini kifo, lakini jambo kuu ni kuamini ufufuo. Hilo ndilo lililotupa maisha mapya.

Katika Matendo ya Mitume 13:33, Biblia inasema, “Ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.” Hii haizungumzii kuzaliwa Kwake kule Bethlehemu, bali kuzaliwa upya katika ufufuo.

Yesu alikuwa mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, ambapo ina maana wa kwanza kuzaliwa kutoka katika kifo cha kiroho. Msalabani, alikufa vifo viwili. Alikufa kiroho kwanza wakati dhambi zetu zilipowekwa juu Yake na akaachwa, akatengwa na Baba. Alilia msalabani “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha” (MARKO 15:34).Pindi hilo lilipotokea, ndipo ilipowezekana kwa Yesu kufa kimwili.


Alipokufa, Alienda kuzimu katika roho, kwa sababu huko ndiko tulikopaswa kwenda sote; Alikwenda kuzimu kwa niaba yetu. Lakini Alikuwa mtu mwenye haki, akizibeba dhambi za wengine. Biblia inatuonyesha jinsi kuzimu, Shetani na pepo wote wa giza walivyoshindana na Yesu ili kumtiisha. Lakini Alizishinda enzi na mamlaka na kuwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani (WAKOLOSAI 2:15)

Yesu alimshinda Shetani hadharani na pepo wa giza na kutoka katika kifo na kuzimu kwa ushindi. Alipofufuka, Biblia inasema Alihesabiwa haki; ufufuo ulikuwa ndio ishara. Kuzaliwa upya katika ufufuo kulimaanisha kwamba hapakuwa na dhambi, hapakuwa na hukumu; deni la dhambi lililipwa kwa kifo Chake, lakini ufufuo Wake katika upya wa uzima ulituletea kuhesabiwa haki (Warumi 4:25).

Ndiyo maana leo, mtu ye yote anayeamini kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zake na kufufuka kwa ajili ya kuhesabiwa haki, anaingia katika upya wa uzima na anakuwa kiumbe kipya: “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima” (Warumi 6:4).

SALA

Baba Mpendwa, ahsante kwa ufufuo wa kitukufu wa Kristo ambao ulituletea kuhesabiwa haki kwa uzima wa milele. Ninatambua ushindi mtukufu Alioupata dhidi ya Shetani na nguvu za giza, Akishinda kifo na kuzimu kwa niaba yangu. Sasa nimeinuliwa pamoja Naye juu sana katika mahali pa ushindi, mamlaka na umiliki milele, katika Jina la Yesu. Amina.

Post a Comment

Previous Post Next Post