YESU ANAKAA NDANI YA YULE
Na
Frt Bruno Mwala OSB
Katika sura ya kwanza tumeweka bayana kuwa Yesu anakaa ndani mwangu, lakini tukifikiri zaidi tunatambua kuwa mimi siishi kama kisiwa. Ninaishi na mwenzangu zaidi hasa ninaishi na wenzangu. Basi wenzangu na mwenzangu yeyote ndio watabeba dhana ya neno yule.
Katika mafundisho ya awali kabisa ya imani yetu tunafundishwa kuwa kwanini Mungu ametuumba na kutuweka duniani? Na majibu yake yakawa Mungu ametuumba na kutuweka duniani ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni.
Katika kipengele cha kumpenda daima huwa tunasisitizwa kuwa hatuwezi kumpenda Mungu tusiyemjua ilhali yule jirani yetu tunayeishi naye hatumtendei wema. Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake kwa hivi kama tukimtendea wema mwezetu ni sawa na kuwa tumemtendea wema Mungu. Kwanini? Kwasababu Yesu anakaa ndani ya Yule.
Bila shaka mahali unakoishi kuna wahtaji wengi sana, labda kutaja japo kwa uchache :
1. Yatima
2. Wajane
3. WaganeWazee
4. Wagonjwa
5. Wafungwa
6. Walemavu mfano wa macho, ngozi, viwete, viziwi.
7. Watu wasio na makazi
8. Wakimbizi
9. Wenye njaa
10. Walio kata tamaa ya maisha
Mimi na wewe tumefanya nini cha pekee ili kuwasaidia hao? Kuna wakati tulikuwa na mazoea ya kuwatembelea watoto wa mitaani mimi na rafiki yangu. Na katika kukutana nao tulikuwa tukiwapatia chakula na kuzungumza nao walau machache.