NOVENA YA ROHO MTAKATIFU -SIKU 02

 *NOVENA YA ROHO MTAKATIFU*


*SIKU YA PILI*


*JUMAMOSI*


*11/05/2024*


*Wimbo*


*NJOO ROHO MTAKATIFU*


/Njoo Roho Mtakatifu, shusha mapaji (kweli) niwe imara x2


Leta nuru ya mwanga wako, ifikie moyoni mwangu x2/


1. Roho mwenye hekima, Roho wa shauri na nguvu


2. Nipatie elimu nitambue nafsi yako


3. Nipatie ibada nikusifu daima milele


4. Roho mwenye uchaji washa moto wako wa mapendo


*kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu Amina*


*ROHO MTAKATIFU ANATUSAIDIA KUENEZA INJILI*


“Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika utawala wa Mungu,” (Yn. 3:5).


Kanisa limepewa na Yesu ujumbe wa kuwaletea watu wote uzima mpya, uzima wa Mungu. Yesu aliwaambia mitume wake: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Nendeni basi mkawafanye watu wa makabila yote kuwa wafuasi wangu. Wabatizeni kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.


 Wafundisheni kuyashika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote mpaka mwisho wa nyakati (Mt.28: 18-20).

Sisi tuliobatizwa tumepata kuwa viungo vilivyo hai vya Mwili wa Fumbo wa Kristu; kwa Kipaimara tumeimarishwa na kuthibitishwa na Roho Mtakatifu. Tumekuwa taifa teule. Tumeshirikishwa ule ukuhani wa Kristu.


 Tumepokea ujumbe wa kueneza utawala wa Mungu. Tunapopokea Sakramenti, na hasa ile Sakmenti ya Ekaristi, tunalisha imani na kuongeza mapendo, ambayo ni msingi wa utume wowote ule. Mapendo yanatuhimiza kueneza utawala wa Mungu na kumpenda Yesu Kristu aliyekuja kuwakomboa wanadamu wote.

Kila aliyebatizwa anao wajibu wa kueneza imani ya Mungu na utawala wake. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kutimiza wito huo.


1. Ee Baba wa mbinguni tunakuomba umpeleke Roho Mtakatifu aliangaze kanisa na kuliongoza, liweze kuwafikishia mataifa yote habari njema ya wokovu.

*W. Twakuomba utusikie*


2. Ee Yesu Mkombozi wetu, umtume Roho Mtakatifu awahimize wakristu wapate kutimiza wajibu wao wa kueneza neno lako popote duniani.

*W. Twakuomba utusikie*


3. Ewe Roho Mtakatifu Mfariji, uamshe katika mioyo ya vijana wengi hamu ya kupenda kulitumikia kanisa lako na kulihudumia taifa lako kwa uaminifu.

*W. Twakuomba utusikie*


4. Ewe mwanga wa mataifa , uwajalie wanafunzi wasikie sauti yako mioyoni mwao, nawe unapowaita wasikose kuisikia sauti yako, wawe tayari kujitoa kwa ajili ya ndugu zao.

*W. Twakuomba utusikie.*


5. Uwasaidie wazazi wawalee vema watoto wao; uwatie moyo katika wito wao, wapate pia kuishiriki vema ile kazi ya kueneza neno lako kwa jirani zao.

*W. Twakuomba utusikie*


6. Ewe Roho Mtakatifu, uwasaidie wakristu wote kueneza habari njema ya wokovu, kwa sala, kwa sadaka na kwa mifano ya maisha yao ya uchaji.

*W. Twakuomba utusikie*


7. Ewe mpaji wa mema, uwajalie waumini mapaji yako saba, wasichoke kulieneza neno lako kwa hekima pasipo hofu.

*W. Twakuomba utusikie.*


*Ongeza nia zako kazi Biashara familia magonjwa masumbuko na yote yanayoitaji mwongozo wa Roho Mtakatifu*


*TUOMBE*


Ee Mungu, unapenda watu wote waokoke, waifikie kweli yako. Tunakuomba uwapeleke wafanyakazi walio wengi na wema katika shamba lako.


Uwajalie kulihubiri neno lako kwa imani kuu ili neno lako lienee na kupokewa na mataifa yote, wapate nao kukujua wewe peke yako Mungu wao, Mungu wa kweli. *Tunaomba hayo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu* *anayeliongoza kanisa lako sasa na milele.*


*W. Amina*


_Kumbuka kusali Litania ya Roho Mtakatifu nilishatuma siku ya kwanza_


*Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu Amina*


Post a Comment

Previous Post Next Post